Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila, amesema upungufu na kutokuboreshwa kwa Mabasi ya Mwendokasi ni vitendo vya kuwahujumu Wananchi wanaotumia usafiri huo ni hujuma dhidi ya juhudi za serikali hususan katika kuleta maendeleo na kuwahudumia Wananchi.
Akiwa Kituoni hapo asubuhi ya leo Julai 24, 2025, katika ziara kwenye Kituo cha Mwendokasi Kimara Mwisho kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu upungufu wa Mabasi hayo, Chalamila amesema hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na kuonya kuwa serikali haiwezi kuvumilia uzembe huo unaojirudia kila mara.
Chalamila amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo takribani miaka Tisa iliyopita, hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa kuboresha au kuongeza Mabasi, hali inayosababisha msongamano na kuchelewesha safari za Wananchi.
Mkuu wa Mkoa pia amehoji ni kwa namna gani mtu binafsi anaweza kutumia gari moja kwa miaka tisa mfululizo bila kufikiria kulibadilisha, achilia mbali magari ya umma yanayohudumia maelfu ya Watanzania kila siku.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameonya kuwa kama wahusika wa usimamizi wa huduma hiyo hawatabadilika na kuchukua hatua madhubuti mara moja, basi atapendekeza wachukuliwe hatua kali, ikiwemo kuondolewa kwenye nyadhifa zao.

