Jeshi la Magereza limetolea ufafanuzi kuhusu muonekano wa Askari kujifunika nyuso (ninja) ambapo limesema Jeshi lina utaratibu wa kupanga matumizi ya mavazi kulingana na mazingira ya kazi au tathmini ya athari za kiusalama kwa Wafungwa, Mahabusu na hata Askari anapotekeleza majukumu ya kazi na kusema kwa namna yoyote mavazi haya hayazuii mwenendo wa kesi Mahakamani wala haki ya Mtuhumiwa.
Taarifa iliyotolewa leo August 02,2025 na Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi, imesema
“Inasisitizwa kuwa Mahabusu au Mfungwa anapokuwa chini ya himaya ya Jeshi la
Magereza ni lazima awajibike kufuata na kutii Kanuni, Miongozo na maelekezo halali anayopewa na Askari ambayo wakati wote yanalenga kuimarisha usalama na kamwe hapaswi kwa namna yoyote kukaidi, anapaswa kutii Sheria bila shuruti”
“Jeshi halitasita kuchukuwa hatua stahiki na kwa wakati katika kukabiliana na viashiria vyovyote vya
changamoto za kiusalama, usalama wa Mahabusu Tundu Lissu utaendelea kuimarishwa wakati wote atakapokuwa chini ya mamlaka ya Jeshi la Magereza”
Hoja ya Askari kuvaa ninja Mahakamani iliibuliwa baada ya Askari hao kuonekana wakivaa ninja Mahakamani kwenye kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

