Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo kwenye kikao maalum kilichofanyika jana August 5, 2025 pamoja na mambo mengine imependekeza majina ya wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Urais wa Zanzibar ambapo kwa upande wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, majina yaliyopendekezwa ni Aaron Kalikawe na Luhaga Mpina.
Kwa upande wa Urais wa Zanzibar Halmashauri Kuu imependekeza jina la Othman Masoud Othman ambaye ndiye Mwanachama pekee aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, Othman Masoud Othman pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa leo August 06,2025 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo, Shangwe Ayo imesema
majina ya Wagombea yaliyopendekezwa yatawasilishwa kwa Mkutano Mkuu Taifa kwa ajili ya kupigiwa kura.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ilipokea na kuridhia hatua ya mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dorothy Jonas Semu kujitoa kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kwenye maelezo yake mbele ya Halmashauri Kuu Dorothy Semu ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo aliieleza Halmashauri Kuu kuwa alichukua hatua hiyo katika kutekeleza wajibu wake wa kiuongozi wa kukiwezesha Chama kutekeleza wajibu wake wa kimapambano wa kuiondosha CCM madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa ya sasa nchini.

