
MSANII wa Wasafi, Zuchu amesema hata kama leo watu watamchukia kwa jinsi alivyo au kwa kuzungumza ukweli, hawezi kuumia hata siku moja kwa sababu anaamini aliyempenda kwa dhati ni mumewe, Diamond Platnumz na mapenzi yake kwake inatosha.
Zuchu alisema hayo baada ya kufanya mkutano na wanahabari na Mwanaspoti lilimvuta pembeni kumuuliza kuhusu kushambuliwa na watu mitandaoni kutokana na mavazi na wimbo wake mpya wa ‘Amanda’ kuja nao kivingine tofauti na vile alivyozoeleka kuimba.
Mwanadada huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa muziki wa taarabu nchini, Khadija Kopa alisema ni ngumu kumridhisha kila mtu, hivyo watu waendelee tu kumchambua kwani anaamini kila kitu ambacho huwa anakifanya kuhusu muziki na mavazi ni sahihi kwa sanaa yake.
“Mimi Mungu kanijalia kuamini kile nachokifanya, tena maneno ya mitandao kwa sasa wala hayaniumizi, siku zote huwezi kufanya kitu na kufanikiwa kumridhisha kila mtu, huo wimbo wa Amanda wapo wanaoupenda na kusifu vyema nimebadili staili ya uimbaji, siyo kuwazoesha mashabiki staili moja ya kuimba, inaboa na kuhusu mavazi yangu wala sijali kabisa na isitoshe mume wangu Diamond akinipenda na akakubaliana na maamuzi yangu kwangu inatosha kabisa siwezi kumridhisha kila mtu,” alisema Zuchu

