Nature

Mpina Ajitokeza Kumtetea Ummy Mwalimu “CCM Wana Sababu Gani Kumfuta Ummy Mwalimu?”

Mgombea urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, amesema hatua ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumfuta aliyekuwa Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, ni kinyume cha haki na inaleta mashaka juu ya mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza leo Agosti 25, mkoani Tanga wakati akiomba udhamini wa wananchi, Mpina alisema wananchi walipaswa kumpima na kumshinda Ummy kwenye sanduku la kura, badala ya chama chake kumwondoa kabla ya uchaguzi.

“Leo hapa Mbunge wenu Ummy naye amefutwa, lakini kwa kumwonea tu. Kwasababu Ummy alitakiwa aje hapa ashindwe na ACT Wazalendo, sio wao kumfuta kule. Kwa mfano, CCM wana sababu gani za kumfuta Ummy?” alihoji Mpina huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Luhaga Mpina, pia ametoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha kuwa haki na sheria vinaheshimiwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi kukiwa na tahadhari nyingi zilizotolewa na Wananchi, Viongozi na Wadau mbalimbali kuhusu kasoro zilizopo katika mfumo wetu wa upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo, hivyo basi, kuna mashaka miongoni mwa wananchi, vyama vya siasa na wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais,” alisema Mpina.

Pia amesisitiza kuwa Tume na Ofisi ya Msajili wanapaswa kutenda haki kwa mujibu wa sheria na kuepuka upendeleo wa aina yoyote, ili kulinda amani na mshikamano wa taifa wakati wa uchaguzi.

Aidha, Mpina amesema ameshuhudia viongozi wa dini kutoka pande zote Kanisa na Misikiti wakiwahamasisha wananchi kuhakikisha taifa linaendelea kudumisha haki na amani katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea uchaguzi.

“Tuna safari ya uchaguzi yenye changamoto, lakini ni lazima changamoto hizo zifuatiliwe na kupatiwa ufumbuzi huku zoezi la uchaguzi likiendelea, Vijana wa ACT Wazalendo wamejipanga kuhakikisha Tanzania inapata uchaguzi wa haki na kidemokrasia,” aliongeza.

Related Posts