Nature

Bokina Faso, Mali na Niger Wajiondoa Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)

Burkina Faso, Mali na Niger zimetangaza kujiondoa mara moja katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wakiitaja “chombo cha ukandamizaji wa ukoloni mamboleo”.

‎Nchi hizo tatu zinazoongozwa na jeshi zilitoa taarifa ya pamoja, zikisema hazitatambua mamlaka ya mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini The Hague.

‎”ICC imejidhihirisha kuwa haina uwezo wa kushughulikia na kushtaki uhalifu wa kivita uliothibitishwa, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa mauaji ya halaiki, na uhalifu wa uchokozi,” viongozi hao watatu walisema.

‎Mahakama hiyo bado haijajibu uamuzi wa nchi hizo tatu, ambazo zote zikiwa na uhusiano wa karibu na Urusi ambayo kiongozi wake Vladimir Putin amepewa hati ya kukamatwa ya ICC.

‎Mataifa hayo matatu yamesema yalitaka kuweka “taratibu za kiasili za uimarishaji wa amani na haki”.

‎Wameishutumu ICC kwa kulenga nchi zisizo na uwezo, wakirejea ukosoaji wa Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye hapo awali aliituhumu ICC kwa kushikilia upendeleo dhidi ya Afrika.

‎ICC ilianzishwa mwaka 2002 ili kufuatilia kisheria kesi za mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na uchokozi.

‎Kwa mujibu wa taarifa Kati ya kesi 33 zilizozinduliwa tangu kuanzishwa kwake, zote isipokuwa moja zilihusisha nchi za Kiafrika. Kujiondoa kwa nchi kutoka ICC kunaanza kutekelezwa rasmi mwaka mmoja baada ya UN kuarifiwa.

‎Vikosi vya kijeshi vinadhibiti Burkina Faso, Mali, na Niger, kufuatia mapinduzi katika nchi za Sahel kati ya 2020 na 2023. Wanaunda wanachama watatu pekee wa Shirikisho la Mataifa ya Sahel.

‎Majeshi yao yamekabiliwa na shutuma za uhalifu dhidi ya raia, huku ghasia zikiongezeka katika eneo hilo dhidi ya makundi ya kijihadi yanayohusishwa na al-Qaeda na Islamic State.

‎Katika hatua nyingine iliyoratibiwa mapema mwaka huu, nchi zote tatu kwa wakati mmoja zilijiondoa katika kambi ya kikanda, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS). Walikuwa wamekataa madai ya ECOWAS ya kuwataka kurejesha utawala wa kidemokrasia.

‎Urusi imeimarisha uhusiano wake na nchi tatu za Sahel katika miaka ya hivi karibuni, ambazo zote zimezidi kutengwa na Magharibi, haswa ukoloni wa zamani wa Ufaransa.

Related Posts