
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amesema kanisa hilo halina mpango wowote wa kukabiliana na Serikali.
Ameeleza hayo leo Oktoba 1, 2025 katika Misa ya Jubilei ya miaka 50 na 25 kwa Mapadre wanaofanya utume Jimbo kuu la Dar es salaam, kwa lengo la kuweka uelewa sahihi katika jamii, ili ifuate msimamo sahihi kutokana na uwepo wa taarifa tofauti.
”Wale wanaohangaika wakidhani kwamba kanisa Katoliki linataka kushindana, kurumbana au kushikana mieleka na Serikali, watambue kwamba sisi hatuna mpango huo” amesema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi amesema waumini wa Kanisa hilo wanapaswa kufuatilia kwa umakini taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii ikiwemo kuhusu Semina ya walei ya kanisa hilo, akikanusha kuwa tangazo kuhusu jambo hilo halikutolewa na ofisi yake
”Naomba nitamke awali ya yote, kwamba tangazo hilo halikutolewa na ofisi yangu, kwahiyo siyo tangazo linalobeba sahihi yangu au lililotangazwa kupitia kwa katibu mkuu. Hilo liwafanye mtambue kwamba siyo tangazo rasmi” amebainisha askofu Ruwa’ichi.

