
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemkabidhi mjane Bi. Alice Haule hati miliki ya nyumba aliyoachiwa na marehemu mume wake huku akimchangia kiasi cha Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuanzia maisha ikiwa ni dhamira ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya kuendelea kuwasaidia Wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii hususan wajane na yatima.
Hayo yamejiri leo Oktoba 20, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo RC Chalamila amempa siku tano Mohamed Mustafa kujisalimisha kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa kuhusiana na sakata la nyumba lililomhusisha na mjane Bi. Alice Haule.
Aidha, RC Chalamila amebainisha kuwa Bwana Mustafa amekuwa na maelezo yasiyoeleweka katika maelezo yake huku akiviagiza vyombo vya Dola kuendelea kumtafuta Mohamed kwa kutumia majina ya Viongozi katika maelezo yake kwa kujinasibu kuwa amekuwa na urafiki wa karibu na Viongozi.
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Dar es Salaam Shukrani Kiyando amesema baada ya kupokea maoni kutoka kwenye timu iliyoundwa kufanya uchunguzi wameamua kuwa haki ya umiliki wa nyumba urudishwe kwa Bi. Alice Haule.
Akizungumza mara baada ya kupokea hati hiyo, Bi. Alice Haule amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wanyonge pamoja na Mkuu wa Mkoa na vyombo vya habari kwa kushirikiana katika kupata haki yake.
Bi Alice amekabidhiwa hati hiyo ya kiwanja Namba 819, kama msimamizi wa mirathi ya marehemu mume wake Justus Rugaibula, ambapo zoezi hilo limefanyika leo Oktoba 20, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Itakumbukwa mapema hivi karibuni Bi Alice alipitia Changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya Kudhalilishwa kwa kutaka kuondolewa kwa nguvu ndani ya nyumba hiyo.

