
BAADA ya kukutwa na hatia katika mashitaka ya rushwa, Rais wa zamni wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani.
Sarkozy alibainika kujinufaisha na fedha alizopokea kwa siri kutoka kwa Serikali ya Libya chini ya Muammar Gaddafi na kuzitumia katika kampeni za urais wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.
Mwanasiasa huyo aliyeikosa hukumu hiyo alisema: “Kama wanataka nilale gerezani, basi nitafanya hivyo, lakini nikiwa sijakata tamaa. Sina hatia.”
Kwa sasa, Sarkozy anatumikia kifungo hicho katika gereza maarufu la La Sante. Ni gereza pekee jijini Paris na lilijengwa mwaka 1867. Hivi karibuni, lilifanyiwa maboresho yaliyochukua miaka minne, kabla ya kufunguliwa rasmi mwaka 2019.
Ndani ya Gereza hilo, mfungwa ana chumba chake chenye jiko, friji, runinga, bafu na choo. Pia, kuna simu maalumu kwa ajili ya mawasiliano.
Aidha, kwa miaka mingi iliyopita imeshuhudia watu maarufu wengi nchini Ufaransa wakipelekwa na kutumikia vifungo vyao.
Mmoja kati ya magaidi waliosakwa vikali na vyombo vya dola katika miaka ya 1970s na 1980, Ramirez Sanchez, maarufu kwa jina la ‘Carlos the Jackal’, aliwahi kuingia La Sante.
Pia, gereza hilo liliwahi kumpokea, Jacques Mesrine, ambaye alisifika kwa mauaji na uvamizi wa benki mbalimbali katika miaka ya 1970.
Kwa miaka ya hivi karibuni, aliyekuwa mlinzi wa Rais Emmanuel Macron, Alexandre Benalla, alipelekwa gerezani huko kuanza kutumikia kifungo cha maisha kwa mashitaka ya kuwapiga waandamanaji.
Wakati huo huo, Sarkozy hatakuwa rais wa kwanza kuingia katika kuta za gereza hilo. Historia ya siasa itamkumbuka kuwa aliyekuwa dikteta wa Panama, Manuel Noriega, alitumikia kifungo chake hapo.
Hata hivyo, kero kubwa ya Gereza la La Sante ni kelele za wafungwa wengine. “Changamoto kubwa iliyopo ni kelele. Usiku, utakuta unaamshwa na kelele za watu,” anasema Didier Schuller, mwanasiasa aliyewahi kutumikia kifungo katika Gereza la La Sante mwaka 2022.

