Chama Cha Mapinduzi yaani CCM kimetoa msimamo wake kutokana na hali ya kisiasa nchini Tanzania kabla, wakati na baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ambapo mgombea wake Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye aliyeibuka mshindi wa kiti cha urais.
Taarifa iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi siku ya leo Jumatano tarehe 5 Novemba, imeeleza wazi kwamba chama hicho kimefanya kikao maalumu cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM Taifa ili kufanya tathimini ya chama chao.
Taarifa iliyotolewa na CCM imeweka wazi kwamba wanatoa shukrani zao za dhati kwa watanzania wote ambao walijitokeza kupiga kura kwa kukichagua chama chao ambacho kimeshinda kwa kishindo kizito kwenye nafasi ya urais.
Taarifa ya CCM imeendelea kueleza kwamba chama hicho kimesikitishwa sana na aina ya vurugu ambazo zilitokea wakati wa uchaguzi ambazo zimesababisha vifo kwa watanzania wengi pamoja na uharibifu wa mali za baadhi ya wafanyabishara ambazo zilichomwa na moto na kundi la waandamanaji.
CCM imelaani vikali vitendo hivyo ambavyo mpaka sasa vimeacha alama mbaya katika taifa letu la Tanzania lakini pia vimeleta mpasuko mkubwa kwa watanzania na kuondoa amani kabisa.
Aidha taarifa hiyo kutoka CCM imeweka wazi kwamba chama hicho kinarudi kukaa chini na kufanya tathimini yake ya kina ili kuona kwa namna bora ya kuanza kuliongoza taifa la Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
Aidha chama hicho kimeitaka serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia kuchukua hatua za muafaka zitakazoifanya nchi yetu ibaki kwenye misingi ya amani na upendo kama ilivyokua kwa miaka kadhaa iliyopita wakati ambao nchi hii ilikuwa inaongozwa na viongozi wengine.
Chanzo: Ukurasa wa Instagram wa CCM.

