Jeshi la Polisi nchini limetoa taarifa kufuatia matukio ya vurugu, uporaji mali na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 nchini na kubainisha kuwa baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, huku msako mkali ukiendelea kuwabaini wengine waliopanga, kuratibu na kutekeleza vitendo hivyo.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi, Dodoma, Tanzania, David A. Misime imeeleza kuwa vurugu hizo zilitokea katika Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya, pamoja na mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa, ambapo ziliripotiwa kusababisha athari kwa uhai na maisha ya watu pamoja na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za watu binafsi.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema kufuatia uchunguzi na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, Jeshi la Polisi linawasaka kwa ajili ya kuwakamata watu kumi (10) na kuwataka kujisalimisha katika vituo vya polisi mara moja watakapoiona taarifa hiyo huku ikitoa orodha ya wanaosakwa ambao ni:-
- Josephati Gwajima
- Brenda Jonas Rupia
- John Mnyika
- Godbless Jonathan Lema
- Achumu Maximillian Kadutu
- Deogratius Cosmas Mahinyila
- Boniface Jacob
- Hilda Newton
- Award Kalonga
- Amaan Golugwa
Katika hatua nyingine,, Jeshi la Polisi limesema kuwa, hatua za kisheria kwa wahalifu ambao tayari wamekamatwa zinaendelea kote nchini na kwamba mnamo Novemba 7, 2025 baadhi wamefikishwa mahakamani
Jeshi la Polisi limeonya kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani ya nchi na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao bila hofu, na kutoa taarifa mapema iwapo watabaini viashiria vyovyote vya uhalifu au uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

