Rais wa Guinea-Bissau aliyeondolewa madarakani, Umaro Sissoco Embaló, amewasili Senegal baada ya kuachiwa na jeshi lililompindua wiki hii.
Uhamisho wake ulifikiwa kupitia mazungumzo ya jumuiya ya ECOWAS, ambayo ilihofia kuongezeka kwa mvutano nchini Guinea-Bissau. Serikali ya Senegal imethibitisha kuwa Embaló aliwasili “akiwa salama” kwa ndege ya Kijeshi iliyomchukua Alhamisi usiku.
Jeshi la Guinea-Bissau tayari limemwapisha kiongozi wa mpito, Jenerali Horta N’Tam, ambaye ataongoza kwa kipindi cha Mwaka mmoja.
Mapinduzi hayo yalitokea siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya Uchaguzi wa Urais na Ubunge, ambayo jeshi limeyazuia na kusimamisha mchakato mzima wa uchaguzi.
Jeshi lilidai lilichukua hatua hiyo kuzuia njama ya kisiasa iliyokuwa na “msaada wa mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya” yenye lengo la kuhatarisha utulivu wa nchi.
Hali ya taharuki iliendelea kutanda katika Mji Mkuu wa Bissau, ambapo maduka na masoko mengi yalifungwa huku Wanajeshi wakilinda mitaa.
Jenerali N’Tam, ambaye ni Mkuu wa Majeshi, alisema jeshi limechukua mamlaka “kuzuia operesheni zilizolenga kutishia demokrasia.” Mara baada ya kuapishwa, alitangaza kufunguliwa tena kwa mipaka ya nchi ambayo ilifungwa wakati wa kutekelezwa kwa mapinduzi.
Jumuiya ya Afrika (AU), ECOWAS na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wamepinga vikali mapinduzi hayo na kutaka kurejeshwa mara moja kwa utawala wa kikatiba.
Guinea-Bissau imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa kwa miaka mingi, ikiwa tayari imepitia takribani mapinduzi 9 au majaribio ya mapinduzi tangu ilipopata uhuru kutoka Ureno mwaka 1974.

