Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa taasisi za kidini likiwemo Kanisa la Ufufuo na Uzima ambapo amemuomba Askofu wa kanisa hilo Josephat Gwajima ajitokeze na kuungana na Serikali katika kujenga umoja wa kitaifa kwa ustawi wa Taifa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Arusha, Dkt. Nchemba amesema viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuunganisha Watanzania na kuhamasisha amani bila kificho.
“Nitamke leo kuwa msamaha uliotolewa ni kwamba kuhusu mliyokuwa mnasema mnamtafuta Askofu Gwajima, nimwelekeze IGP na Jeshi la Polisi mwacheni aendelee na ibada zake. Ajitokeze tushikamane turejeshe umoja wa kitaifa,” amesema Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa mazungumzo ya kindugu pia yamefanyika na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) pamoja na taasisi nyingine za kidini ili kuhakikisha umoja, mshikamano na amani ya nchi vinaimarishwa.
“Nawaomba viongozi wote wa kidini, kimila na makundi mbalimbali, twendeni pamoja kuhamasisha Tanzania kuwa nchi ya amani,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.

