Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amewasihi Watanzania kwa ujumla kutokushabikia vurugu kabisa kwakuwa vurugu zina gharama yake.
Akiongea kwenye mkutano wa RC Chalamila na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo December 05,2025, Muliro amesema “Polisi tunatambua kwamba Serikali hii ni ya Watu na tunatambua tunawatumikia Watu, tunatambua kuwa ili ulinde amani ambalo ni jukumu letu Watu wanatakiwa kuzitii sheria, pamoja na uhuru wa maoni sheria inatukumbusha pia mipaka”
“Polisi jukumu lake kubwa ni kuhakikisha Watu wanaishi kwenye mazingira yasiyo na hofu na Watu walindwe, nikubaliane na lile ambalo Wahariri mmetukumbusha la kuhakikisha mnakuwa salama ili mzipate taarifa vizuri na tunaamini mngezipata vizuri taarifa tungeepuka taharuki zilizojitokeza kwahiyo tukiri hilo tutalitekeleza ili mzunguke mueleze hali halisi ya mambo na wala hatutaki mtupendelee”
“Mwisho niwaambie Wanahabari hii Nchi ni yetu, tusishabikie hata kidogo tukaenda kwenye mrengo wa kufanya tuwe kwenye vurugu, vurugu zina gharama, kuna mambo ya kujaribu lakini kuna mambo haupaswi kujaribu maana chochote kikitokea wewe na Mimi mazingira yetu hayatokuwa mazuri”
“Sisi tutaendelea kusimamia sheria kuona Dar es salaam inakuwa salama na Wahariri na Wananchi wengine kwa ujumla mtekeleze majukumu yenu bila hofu” – Muliro.

