WAKATI kikosi cha Singida Black Stars kikitarajiwa kushuka uwanjani leo jioni kuvaana na TRA United, zipo taarifa kuwa kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho yupo katika rada za wababe wa Morocco, Raja Athletic wanaonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.
Aucho alijiunga na Singida kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Yanga alikokuwa amecheza kuanzia 2021-2025. Chanzo kimeeleza endapo kama Aucho atafanikiwa kujiunga na Raja Athletic ataungana na Fadlu, kocha ambaye wakati akiwa Simba, Aucho alikuwa anakipiga upande wa pili kwa watani, Yanga.
“Kocha Fadlu ndiye anayemhitaji Aucho na mazungumzo yanaendelea na ofa aliyowekewa mezani ni nono ingawa siwezi kusema ni kiasi gani. Aucho amebakiza mkataba wa miezi sita anaruhusiwa kuzungumza na timu zingine kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa ikiwemo kuzungumza na viongozi wa Singida Black Stars.”

