Mahakama ya Paris nchini Ufaransa imeagiza timu ya Paris St Germain (PSG), kumlipa Kylian Mbappe Euro Milioni 60 (Shilingi Bilioni 175 za Tanzania ) za Mshahara na bonasi ambazo hazikulipwa, hatua iliyopelekea kuwa moja ya migogoro mikali zaidi katika soka la Ufaransa.
Uamuzi huo ulifuata miezi kadhaa ya mvutano wa Kisheria baada ya Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa kuipeleka PSG Mahakamani, akidai malipo aliyosema yalizuiwa kwa miezi ya Aprili, Mei na Juni 2024, muda mfupi kabla ya kuondoka katika klabu hiyo ya Ligue 1 na kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa bure.
“Tunaridhishwa na uamuzi huo. Hii ndicho unachoweza kutarajia pale malipo ya Mishahara hayajalipwa,” alisema Wakili wa Mbappe, Frederique Cassereau, kwa waandishi wa habari.
Mahakama ilibaini kwamba PSG haikumulipa Mbappe Mshahara wa miezi mitatu, bonasi ya maadili (ethics bonus) na bonasi ya kuingia mkataba (signing bonus) kama ilivyokubalika chini ya mkataba wake wa ajira.
