Jeshi la Polisi Lazibitisha Kumkamata Kweka Kwa Makosa Haya

Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kumkamata na kumshikilia Thadey Sabinus Kweka kwa tuhuma za makosa ya jinai ikiwemo uchochezi, likieleza kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa siku ya Jumatatu Desemba 29, 2025 na Msemaji wa Jeshi hilo, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, DCP David Misime, mtuhumiwa huyo alikamatwa usiku wa Desemba 28, 2025, mkoani Kilimanjaro, na kwa sasa anashikiliwa kwa ajili ya kuendelea na taratibu za kisheria.

“Taratibu za kukamilisha ushahidi ikiwa ni pamoja na kupata maelezo yake juu ya tuhuma hizo unaendelea ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata”, imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa ya Polisi imekuja saa chache baada ya kusambaa kwa madai katika mitandao ya kijamii yakidai kuwa Thadey Kweka, Mtanzania anayeishi nchini Marekani na akitajwa kama mwanaharakati wa demokrasia na haki za binadamu, alikuwa ametekwa nyumbani kwake Moshi na watu waliodaiwa kuwa na silaha.

Imeelezwa kuwa Thadey Kweka aliwasili nchini Tanzania wiki iliyopita kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, pamoja na kuhudhuria harusi ya ndugu yake mkoani Kilimanjaro.

Jeshi la Polisi halijatoa maelezo ya kina juu ya mazingira ya kukamatwa kwake zaidi ya kueleza kuwa alikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria, huku likisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Related Posts