Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe, Mhashamu Eusebio Kyando, amesema baadhi ya vijana wanapoteza mwelekeo wa imani kwa kuyumbishwa na tamaa ya umaarufu, pesa na mahitaji ya maisha, akionya kuwa hali hiyo inasababisha wengine hata kuukana wazi Ukristo wao.
Askofu Kyando ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia Teule ya Karoli Lwanga Nzengelendete, mkoani Njombe, akirejea mijadala inayoendelea mitandaoni kuhusu madai yanayohusisha vijana Wakatoliki kumlalamikia Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima.
Amesema ameshuhudia kupitia mitandao ya kijamii madai yanayodai kuwa vijana Wakatoliki wanamshtaki Padri Dkt. Kitima kwa Papa, akieleza kuwa kauli hizo zinaonesha upungufu wa uelewa wa mifumo ya Kanisa na ni ishara ya vijana wanaotafuta umaarufu kwa gharama ya imani yao.
Kauli ya Askofu Kyando inakuja siku chache baada ya waumini wawili wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kuwasilisha barua rasmi kwa Balozi wa Vatican nchini (Apostolic Nuncio), Askofu Mkuu Angelo Accattino, wakiomba kufanyika kwa mapitio ya kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, mmoja wa waandishi wa barua hiyo, Stanslaus Nyakunga, alisema yeye pamoja na Elia Phaustine walichukua hatua hiyo baada ya kuwepo kwa malalamiko na mijadala ya muda mrefu ndani ya jamii na miongoni mwa waumini kuhusu kile walichokitaja kuwa ni kuhusishwa kwa Padri Dkt. Kitima na masuala ya kisiasa.
Nyakunga alieleza kuwa mitazamo hiyo imekuwa ikidai kuwa Padri Dkt. Kitima amekuwa akionekana kuingilia au kushiriki katika migogoro ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa namna inayotafsiriwa kuwa ya wazi, hali ambayo, kwa mujibu wao, haijawahi kujitokeza kwa kiwango kama hicho kwa vyama vingine vya siasa.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa barua hiyo haikulenga kutoa hukumu, kumshambulia binafsi Padri Dkt. Kitima wala kuhoji dhamira yake ya kichungaji, bali ilikuwa ni ombi rasmi la kikanisa lenye lengo la kulinda taswira, umoja na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania.
Source ; Jambo TV
