
Afisa wa juu wa kupambana na ugaidi nchini United States, Joe Kent, amejiuzulu wadhifa wake akipinga wazi vita dhidi ya Iran, huku akimtaka Rais Donald Trump “kubadili mwelekeo” wa sera hiyo.
Kent, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC), alitoa uamuzi huo kupitia barua aliyochapisha kwenye mtandao wa X.
Katika barua yake, Kent alisisitiza kuwa Iran haikuwa na tishio la haraka kwa Marekani, akidai kuwa:
Vita hiyo ilianzishwa kutokana na shinikizo kutoka Israel na ushawishi wa “lobby yenye nguvu” nchini Marekani.
Aliongeza kuwa taarifa zilizotolewa zilimshawishi rais kuamini kuwa Iran ilikuwa karibu kushambulia –jambo alilolitaja kuwa si la kweli.
Utawala wa Donald Trump ulijibu haraka, ukisema kuwa ulikuwa na ushahidi wa kutosha unaoonyesha Iran ilikuwa inapanga shambulio dhidi ya Marekani.
Hata hivyo, kauli za Kent zimeibua mjadala mkali ndani ya siasa za Marekani, hasa kutokana na uzito wa nafasi aliyokuwa nayo.
Shirika la Anti-Defamation League lilimkosoa Kent, likisema baadhi ya madai yake yanafanana na “mitazamo ya chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism)”.
Vilevile, kundi la ushawishi wa kisiasa American Israel Public Affairs Committee lilisambaza kauli hiyo, likionesha kuunga mkono ukosoaji huo.
Kujiuzulu kwa Joe Kent kunamfanya kuwa mmoja wa maafisa wakubwa zaidi ndani ya utawala wa Trump kupinga hadharani hatua ya Marekani kushirikiana na Israel katika mashambulizi dhidi ya Iran.
