Klabu ya Simba inajiandaa kuingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka huu wa 2026, huku hali ya taharuki ikitanda juu ya nani atachukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa, Murtaza Mangungu. Majina matano ya vigogo wenye ushawishi mkubwa yameanza kupigiwa chapuo, yakiongozwa na sura zinazofahamika kama Moses Kaluwa, Mohamed Soloka, na Swedy Mkwabi, huku kukiwa na shinikizo kubwa la kutaka mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu.
Katikati ya vuta ni kuvute hiyo, jina la aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Barbara Gonzalez, limeibuka upya na kuleta msisimko wa kipekee miongoni mwa wanachama.
Taarifa za kiintelejensia zinaeleza kuwa kundi la wanachama waandamizi huko matawini tayari limeanza kusuka mikakati mizito ya siri ili kumuandalia mazingira ya ushindi, huku Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, naye akitajwa kwenye orodha hiyo ya watia nia wanaoweza kuleta upinzani mkali.
​Uchaguzi huu unatazamwa kama kigezo muhimu cha mustakabali wa Simba kibiashara na kimichezo, kwani wanachama wamekuwa wakipiga kelele kutaka uongozi utakaoweza kurudisha heshima ya klabu hiyo katika ramani ya soka la Afrika. Wakati mchakato wa mikakati ukizidi kupamba moto huko matawini, macho ya wanasimba wote sasa yameelekezwa kwenye sanduku la kura ili kuamua ni nani kati ya vigogo hawa watano atakayekabidhiwa jukumu la kuivusha timu hiyo.
