
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka vijana na wanafunzi nchini kufanya utafiti kabla ya kuchukua hatua zinazoendeshwa na hisia, akisema kuna juhudi kubwa za kutengeneza chuki dhidi ya Serikali na viongozi wake hasa kuelekea matukio muhimu ya kitaifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam alipokutana na wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chalamila amesema katika miezi ya karibuni kumekuwepo mbinu za kuwapotosha vijana kupitia mitandao ya kijamii, ikiwemo kusambazwa picha za magari yanayodaiwa kumilikiwa na watoto wa viongozi ili kuibua chuki isiyo na msingi. Amesema mara nyingi taarifa hizo hazina ukweli, na hutumiwa kuandaa mazingira ya kuamsha hasira na chuki ndani ya jamii.
Chalamila amesema chuki kama hizo hazina tija kwa taifa, na mara nyingi hutumiwa kuvuruga taswira ya serikali mbele ya wananchi wake. Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuelewa madhara ya kuchoma miundombinu au kufanya vurugu, kwani vitendo hivyo huishia kuharibu rasilimali wanazozitegemea kwa maendeleo yao ya baadaye.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo rasmi ya uwakilishi wa wanafunzi kutoa hoja zao, badala ya kujiingiza katika misukumo ya kihisia. Amesema serikali iko tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za wanafunzi kupitia viongozi wao wa vyuo, baraza la wanafunzi na uongozi wa kitaaluma, akisisitiza kuwa “hasira ziende kwenye vitabu” ili kuleta hoja zenye mashiko.

