Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka Duniani wa FIFA, Arsène Wenger, ametoa kauli nzito baada ya fainali ya AFCON 2025, akigusia mazingira magumu ya kisaikolojia ambayo wenyeji Morocco walikabiliana nayo. Wenger alidai kuwa bara zima la Afrika lilionekana kuwa kinyume na Morocco katika hatua za mwisho za mashindano hayo, jambo ambalo mara nyingi hutokea kwa timu mwenyeji inapokuwa na nguvu kubwa. “Afrika nzima ilikuwa dhidi ya Morocco. Unawezaje kufanikiwa wakati bara zima liko kinyume nawe?” alihoji Wenger, akionyesha kushangazwa na uimara wa timu hiyo licha ya shinikizo kubwa la nje.
Licha ya changamoto hizo, “Le Professeur” hakuacha kuipongeza Morocco kwa ukomavu wa kimichezo na uandaaji wa kiwango cha juu ulioshuhudiwa katika michuano hiyo ya 35 ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Wenger alipongeza nidhamu na moyo wa ushindani (sportsmanship) ulioonyeshwa na Morocco muda wote wa mashindano, akitaja kuwa shirika na miundombinu ilikuwa ya “ajabu na isiyoaminika.” Sifa hizi kutoka kwa Wenger zinazidi kuimarisha hadhi ya Morocco kama taifa linaloweza kuandaa matukio makubwa ya soka ulimwenguni, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia 2030.
Kauli hii ya Wenger inakuja wakati ambapo mchezo huo wa fainali dhidi ya Senegal ulitawaliwa na hisia kali na migogoro ya uwanjani, hali iliyopelekea Rais wa FIFA, Gianni Infantino, na kocha wa Morocco, Walid Regragui, kulaani vurugu zilizotokea. Hata hivyo, tathmini ya Wenger inatoa mtazamo tofauti kwa kuthamini ubora wa soka na uwezo wa Morocco kuhimili dhoruba za kisaikolojia. Kwa Wenger, AFCON 2025 imekuwa kielelezo cha ukuaaji wa soka la Afrika, hasa kwa kuona makocha wazalendo wakiongoza timu zote nne zilizofika nusu fainali.
