Baba Askofu Rev. Dr. Benson Bagonza (PhD), Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, amesema kumekuwa na msemo maarufu kuwa vijana “wameshawishiwa” na watu waishio nje ya nchi, jambo ambalo kwa mujibu wake linaonyesha kuwa vijana hawajalazimishwa, kuburuzwa, kutishwa wala kuhongwa bali wameshawishiwa kwa hoja.
Kupitia andiko lake kwenye mitandao ya kijamii, Bagonza amesema kuwa naye ameshawishika kuwashauri watawala watumie ushawishi kuzungumza na vijana, akibainisha sababu kadhaa zinazohitaji kuzingatiwa na mamlaka.
Amesema kwamba kuandamana ni haki ya kikatiba na hivyo Serikali haitakiwi kutumia nguvu kuvunja Katiba, bali kutumia busara na ushawishi katika kushughulika na madai ya vijana.
“Tuwashawishi vijana waahirishe haki yao ya kikatiba na siyo kuwatisha,” ameandika.
Ameeleza kuwa kabla ya Oktoba 29 kulitumika vitisho kuzuia maandamano, lakini vitisho hivyo havikuleta matokeo yaliyotarajiwa, akionya kuwa ushauri wa kutumia vitisho haupaswi kuendelezwa kwa kuwa “haukusaidia”.
Aidha, amesema wakati viongozi mbalimbali wa kitaifa wanazunguka kuongea na makundi ya wananchi na kujaribu kuyashawishi, bado baadhi ya lugha za kibabe kutoka kwa polisi na baadhi ya watawala zinaathiri juhudi hizo kwa kuwavunja moyo vijana.
Katika hoja nyingine, Bagonza amesema kuwa kabla ya Oktoba 29, mamlaka zilisisitiza zaidi wimbo wa amani na kukataa kusikiliza hoja zinazohusu haki, jambo ambalo amesema halikuleta matunda mazuri.
“Kabla ya Oktoba 29, tulitumia vitisho kuzuia maandamano. Vitisho havikusaidia. Mganga aliyetudanganya kuwa vitisho vinafaa yeye ndiye hafai. Tusiendelee kumuamini. Sasa waimbieni wananchi wimbo wa HAKI japo kuwapa matumaini,” amesema.
Amefafanua pia kuwa Tanzania ilitia sahihi mkataba wa haki za watoto unaowapa watoto haki ya kusikilizwa, na matokeo yake ni kwamba taasisi nyingi, zikiwemo familia, shule, mahekalu, polisi na serikali, zimekuwa zikiwaogopa zaidi watoto kuliko kuwaongoza.
“Tulitia sahihi mkataba wa haki za watoto. Haki yao moja kubwa ni kusikilizwa. Matokeo ya mkataba huo ni kuwa wazazi, walimu, polisi, mahekalu na serikali zote zinaogopa watoto. Watoto wanaogopwa lakini hawaogopi Wakikuhurumia watakunywa sumu kuliko kufuata ubabe wako.

