Klabu ya Azam FC imeonyesha nia ya dhati ya kumsajili kiungo mkabaji wa Yanga SC, Aziz Andabwile (22), ikijiandaa kutuma ofa rasmi katika dirisha dogo la usajili la Januari.
Kwa mujibu wa taarifa, Azam imekuwa ikimfuatilia Andabwile kwa muda sasa, ikivutiwa na uwezo wake wa kukaba, kutengeneza ulinzi wa kati na uthabiti wake katika kutuliza mchezo. Klabu hiyo inaamini kuongeza mchezaji wa aina yake kutaimarisha safu yao ya kiungo kuelekea mzunguko wa pili wa ligi.
Andabwile alianza msimu kwa kiwango cha juu chini ya kocha Romain Folz, lakini tangu kutimuliwa kwa kocha huyo, kiungo huyo ameonekana kupoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Yanga jambo linalodaiwa kuchangia kutokuwa kwake na furaha ndani ya timu.
Hali hiyo imefanya Azam kuona nafasi ya kunufaika na hali ya mchezaji huyo, huku ikisemekana tayari inaandaa ofa ambayo inaweza kuwashawishi mabosi wa Yanga kukubali mazungumzo.
Hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka pande zote mbili, lakini iwapo dili hilo litakamilika, Andabwile anaweza kuwa moja ya usajili mkubwa kwenye dirisha dogo la Januari.

