Kampuni ya teknolojia ya Marekani, Astronomer, imetangaza kujiuzulu kwa Afisa Mtendaji Mkuu wake, Andy Byron, kufuatia kusambaa kwa video inayomuonesha akimkumbatia mchepuko katika tamasha la Coldplay.
Tukio hilo lilinaswa kwenye skrini kubwa ya Gillette Stadium mjini Foxborough, Massachusetts, na kuoneshwa kwa hadhira ya maelfu ya watu. Mara baada ya sura zao kuonekana hadharani, wawili hao walijificha kwa haraka – jambo lililoibua hisia kali na uvumi mitandaoni. Mwimbaji wa Coldplay, Chris Martin, alitania kwa kusema: “Huenda wana uhusiano wa siri, au ni waoga sana.”
Watu waliotajwa kwenye video hiyo wanadaiwa kuwa ni wakurugenzi wa Astronomer – Andy Byron na Kristin Cabot, afisa wa rasilimali watu. Hata hivyo, hakuna yeyote kati yao aliyethibitisha kuwa ndiye aliyerekodiwa katika video hiyo.
Ijumaa, Astronomer ilitoa taarifa rasmi ikithibitisha kuwa Byron amejiuzulu, huku uchunguzi wa ndani ukiendelea. Ingawa taarifa hiyo haikutaja moja kwa moja video hiyo, kampuni ilisisitiza kuwa taarifa zinazodai Byron alitoa kauli binafsi ni za uongo, na pia ilikanusha kuwa kuna mfanyakazi mwingine aliyekuwa kwenye tukio hilo.
Tangu kuanzishwa kwa Astronomer, uadilifu na uwajibikaji vimekuwa nguzo zetu kuu. Viongozi wetu wanatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa katika maadili na mwenendo, ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa sasa, mwanzilishi mwenza na Mkuu wa Bidhaa wa kampuni hiyo, Pete DeJoy, ameteuliwa kuwa kaimu Afisa Mtendaji Mkuu.

