Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusu Mauaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu yaliyotekelezwa katika Uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba nchini Tanzania.
Taarifa zilizopokelewa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo mbalimbali nchini Tanzania zinaonyesha kuwa mamia ya waandamanaji na watu wengine wameuawa, na idadi isiyojulikana kujeruhiwa au kukamatwa. Ofisi hiyo haijaweza kuthibitisha kwa uhuru idadi ya vifo kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa mtandao kulikofuata baada ya uchaguzi.
“Ripoti za familia zinazohangaika kutafuta wapendwa wao kila mahali, wakitembelea kituo kimoja cha Polisi baada ya kingine na hospitali moja baada ya nyingine, ni za kusikitisha sana. Ninatoa wito kwa Mamlaka za Tanzania kutoa taarifa kuhusu hatma na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa familia zao ili wapate kupewa maziko ya heshima,” alisema Türk.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amezitaka Mamlaka za Tanzania kuchunguza tuhuma hizi nzito za ukiukaji wa haki za binadamu kwa uwazi na kwa kina, na kuwawajibisha wote waliohusika.
Pia alitoa wito tena kwa Mamlaka kuwaachilia bila masharti viongozi wote wa Upinzani waliokamatwa kabla ya Uchaguzi Mkuu, akiwemo Kiongozi wa Chama cha Upinzani Chadema, Tundu Lissu, pamoja na watu wengine wote waliokamatwa tangu siku ya uchaguzi. Inaripotiwa kuwa zaidi ya watu 150 wamekamatwa tangu kura kupigwa.
Wengi wao, wakiwemo Vijana, wameripotiwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini.
By Maulid Kitenge

