Bwege Atimka ACT Wazalendo na Kujiunga Chama Hichi

Mwanasiasa machachari na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Senior Selemani Said Ally Bungara maarufu kama Bwege, ametangaza rasmi kujiondoa katika chama cha ACT Wazalendo kuanzia Februari 18, 2026. Taarifa hiyo ameitoa kupitia ujumbe wake kwa umma, akieleza kuwa uamuzi huo umetokana na tafakuri ya muda mrefu na tathmini binafsi ya mwenendo wa kisiasa ndani ya chama hicho.

Bwege ameeleza kuwa ameuchukua uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe kama mtu huru, baada ya kugundua kuwa ACT Wazalendo si “rafiki sahihi” katika safari yake ya kisiasa kama alivyokuwa akiamini hapo awali. Amesema kuwa mwelekeo wa sasa wa chama hicho ni tofauti na matarajio yake, jambo lililomfanya kuona ni vyema kutafuta jukwaa jingine la kuendeleza harakati zake za kisiasa.

Katika maelezo yake, Bwege ambaye anafahamika kwa misimamo yake thabiti na lugha ya mvuto jukwaani, amebainisha kuwa tofauti za kimtazamo na kimkakati zimekuwa sababu kuu ya kujiondoa kwake. Amesisitiza kuwa hatua hiyo haijatokana na shinikizo lolote bali ni matokeo ya uamuzi wa busara alioufikia baada ya kupitia safari yake ndani ya chama hicho.

“ACT Wazalendo si rafiki sahihi kwangu, nilivyofikiria ni tofauti na nilivyohisi. Kuanzia sasa mimi si mwanachama wa ACT Wazalendo tena kuanzia tarehe 18/2/2026. Mengine nitaongea baadaye. Ninategemea kushirikiana na kulitumia jukwaa la CHADEMA katika siasa za kudai demokrasia na maendeleo ya taifa langu nilipendalo – Tanzania,” ameandika Bwege katika taarifa yake.

Kupitia kauli hiyo, ameweka wazi nia yake ya kushirikiana na CHADEMA kama jukwaa jipya la kisiasa, akieleza kuwa anaona chama hicho kinaendana zaidi na maono na malengo yake katika kudai demokrasia na maendeleo ya taifa. Hata hivyo, hajaeleza kwa kina iwapo tayari amejiunga rasmi na chama hicho au kama bado yupo katika hatua za mashauriano.

Hatua ya Bwege kujiondoa ACT Wazalendo imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa siasa na wananchi, hasa ikizingatiwa historia yake ya kuwa mbunge na mchango wake katika mijadala ya kisiasa nchini. Wengi wanasubiri maelezo zaidi aliyosema atayatoa baadaye ili kufafanua sababu za kina zilizopelekea uamuzi huo pamoja na mwelekeo wake mpya wa kisiasa.

Kwa sasa, macho na masikio ya wadau wa siasa yameelekezwa kwake kusubiri hatua zinazofuata katika safari yake ya kisiasa baada ya kuhitimisha rasmi uanachama wake ndani ya ACT Wazalendo

Related Posts