Chaba, Dudukwe Wanajulikana Dunia Nzima, Walindwe -Makalla

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameziagiza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na Baraza la Madiwani kuhakikisha jamii ya Wahadzabe inalindwa, na maeneo yao hayavamiwi wala kuharibiwa, ili kuzuia kuhama kwao kutoka Wilaya hiyo.

Akizungumza leo, Jumatano Januari 7, 2025, katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Makalla amesema jamii ya Wahadzabe ni miongoni mwa Vivutio vikubwa vya utalii wa kiutamaduni kutokana na kuendeleza maisha yao ya asili, jambo linalowavutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.

“Leo ndugu zetu Wahadzabe wanaweza kuanza kutoweka kama mazingira yao yakiendelea kuwa hatarini. Kama ilivyo kwa jamii zinazohama zihitajiapo malisho, kwao pia usalama au ukosefu wa chakula unaweza kuwafanya wahame. Madiwani mnawajibika kuwalinda ili wapate mahitaji muhimu. Kama kuna sheria zinapuuzwa, nendeni mkazisimamie, mkawalinde na mlinde maeneo yao,” alisema Makalla.

Amefafanua kuwa uharibifu wa mazingira wanayoishi Wahadzabe, jamii inayojulikana kwa kuhifadhi urithi wake wa asili, unaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watalii wanaowatembelea kwa lengo la kujifunza kuhusu maisha yao ya kipekee katika eneo la Eyasi, Karatu.

Related Posts