Nature

Chadema Wazuiliwa Kumuona Tundu Lissu Gereza la Ukonga

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kuwa Serikali kupitia Jeshi la Magereza limezuia Viongozi wa Chama hicho kumtembelea na kumuona Mwenyekiti wake ambaye ni Tundu Antipas Lissu katika Gereza la Ukonga.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi CHADEMA, Brenda Rupia imeeleza yafuatayo “katika siku za karibuni, Viongozi wa Chama akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Katibu Mkuu John Mnyika wamezuiwa kuingia Gereza la Ukonga kumwona Mwenyekiti Lissu”

“Leo Novemba 30, 2025, Mhe. Mnyika alipofika gerezani akaambiwa na Askari wa Magereza kuwa kuna maelekezo ya kutoruhusu Kiongozi yoyote wa CHADEMA kuonana Mhe. Lissu, hatua hii inaashiria zuio lisilo la kawaida linalokiuka haki za msingi za Mahabusu akiwa Gerezani la kutembelewa na kuonwa na Ndugu na Jamaa zake”

“CHADEMA inachukulia hatua hii kama uvunjaji wa haki za msingi za wafungwa na mahabusu na matumizi ya vyombo vya dola kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani, Chama kinataka Jeshi la Magereza litoe maelezo kwanini wanazuia Mhe. Lissu asionane na viongozi wenzake, Wadau wa ndani na nje ya nchi kufuatilia mwenendo huu hatari kwa mustakabali wa demokrasia na maisha ya Mhe. Lissu, CHADEMA itachukua hatua za kisheria, kisiasa na kidiplomasia kuhakikisha haki za Mhe. Lissu na viongozi wa chama hazikiukwi”

Related Posts