Clement Mwandambo Aachiwa na Polisi Kwa Dhamana

Mwalimu wa Shule ya Awali ya Saint Clemence jijini Mbeya, Clemence Kenan Mwandambo, ameachiwa kwa dhamana jioni ya leo, Novemba 27, 2025, na atatakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya kesho kwa ajili ya kuendelea na taratibu za uchunguzi.

Mwandambo, mkazi wa Uzunguni “A” Mbeya, alikamatwa Novemba 21, 2025 majira ya saa 5:20 asubuhi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kutoa na kusambaza maneno ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii, ikiwemo Facebook na Instagram. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya alithibitisha kumshikilia mtuhumiwa Novemba 22, 2025, akibainisha kuwa uchunguzi dhidi yake unaendelea.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) @thrdcoalition ulitoa wito kuomba mtuhumiwa apatiwe dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kupitia taarifa yao ya Novemba 22, 2025, THRDC ilieleza kuwa imewatuma mawakili wake mkoani Mbeya, wakiongozwa na Wakili Philip Mwakilima, kufuatilia hatua zote za kisheria, kumwakilisha Mwandambo na kulinda haki zake kama raia na mtoa maudhui mtandaoni.

Hata hivyo, wakati Wakili Mwakilima alipotembelea kituo cha polisi kumwona mteja wake, hakuruhusiwa kuonana naye. Alielezwa kuwa Mwandambo tayari amehojiwa na kwamba upelelezi bado unaendelea, hivyo suala la dhamana lilikuwa bado halijafikiwa.

Related Posts