Crescentius Magor Afunguka Matatizo Yanayoiandama Timu ya Simba Kwa Sasa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Crescentius Magori,leo amevunja ukimya na kutoa ufafanuzi wa kina juu ya hali ya kiufundi inayoiandama klabu hiyo kwa sasa. Katika kauli yake iliyojaa msisitizo, Magori amewatuliza mashabiki wa “Wekundu wa Msimbazi” akibainisha kuwa timu hiyo haipo kwenye hali mbaya kama inavyovuma mitaani, bali inapita katika kipindi cha mpito cha kiufundi.

Magori ameeleza kuwa moja ya sababu kuu zilizoyumbisha utulivu wa timu ni mabadiliko ya ghafla katika benchi la ufundi. Alibainisha kuwa kuondoka kwa kocha aliyeandaa timu tangu mwanzo wa msimu na kuingia kwa mwalimu mwingine ambaye hakuwa na vigezo vilivyotarajiwa, kuliathiri mfumo wa uchezaji.

“Kiufundi, timu iliyumba kwa sababu kocha aliyekuwa amezindua msimu aliondoka, na kisha kuja kocha ambaye hajakidhi vigezo,” alisema Magori. Hali hii ilisababisha wachezaji kuhitaji muda zaidi wa kuelewa falsafa mpya katikati ya mashindano.

Mbali na benchi la ufundi, Magori alitaja wimbi la majeraha kwa wachezaji tegemeo kama sababu nyingine ya kusuasua kwa matokeo. Alitolea mfano beki wa kati aliyeumia kwenye Ngao ya Jamii, kufuatiwa na kipa namba moja, pamoja na beki mwingine wa akiba aliyepata majeraha mara tu alipopewa nafasi. Pengo la wachezaji hawa wa muhimili wa ulinzi limekuwa likionekana katika mechi za hivi karibuni, jambo ambalo limeleta hofu isiyo na msingi kwa wafuasi.


Licha ya malalamiko makali kutoka kwa mashabiki, Magori amewataka wana-Simba kutazama takwimu badala ya hisia. Alisisitiza kuwa klabu hiyo imeshacheza mechi tano za ligi na kupoteza mchezo mmoja tu, jambo ambalo ni la kawaida katika soka la ushindani.

“Lakini maneno hayo yanakuzwa. Tumeshacheza mechi tano za ligi na kupoteza mechi moja tu, lakini kelele zimepandwa kama mwisho wa dunia,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Magori amewahakikishia mashabiki kuwa uongozi unafanyia kazi mapungufu yote yaliyoonekana ili kuirejesha timu katika makali yake ya awali. Amewataka wanachama kuwa na uvumilivu wakati timu ikijisuka upya, akiamini kuwa kurejea kwa wachezaji majeruhi na utulivu wa benchi la ufundi kutaleta mapinduzi makubwa uwanjani.

Kwa kauli hiyo, Magori ameweka wazi kuwa Simba bado ipo kwenye mbio za ubingwa na dhoruba inayopita sasa ni sehemu ya mchezo ambayo itadhibitiwa hivi karibuni.

Related Posts