MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ametoa kauli kuhusu uvumi wa kufungwa kwa ukumbi wa Tanzanite uliopo Kimara Korogwe, akibainisha kuwa ukumbi huo umesajiliwa kwa ajili ya shughuli za biashara na si kwa ajili ya ibada.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam Msando amesem ukumbi wa Tanzanite ulitumiwa na Kanisa la ABC kutoka Shinyanga kwa ajili ya semina ya kidini ambayo ilimalizika siku ya Ijumaa.
Ameeleza kuwa yeye binafsi alifika ukumbini hapo na kuzungumza na viongozi wa dini waliokuwepo, bila kuchukua hatua yoyote kwa kuwa shughuli iliyoombewa matumizi ya ukumbi ni semina.
Pia Msando ameonya dhidi ya waumini wa Kanisa la Gwajima, ambao amesema wamekuwa wakitumia makanisa na maeneo mengine kwa mikusanyiko isiyo rasmi baada ya kanisa lao kufungiwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu.
“Ukumbi wa Tanzanite haukusajiliwa kwa ajili ya ibada. walioomba semina ni Kanisa la ABC, siyo waumini wa Gwajima. kwa hiyo mikusanyiko ya aina hiyo ni marufuku,” amesema Msando.
Ameongeza kuwa waumini waliotakiwa kufika ofisini kwake hawakufanya hivyo, badala yake walienda mahakamani na kisha kuhamia katika kanisa lingine bila ruhusa, jambo ambalo amesema ni kinyume cha sheria.
“Haki ya kuabudu ipo, lakini lazima ifuate utaratibu. Viongozi wa Gwajima wasithubutu kufanya mikusanyiko isiyo rasmi ndani ya Wilaya ya Ubungo,” amesisitiza.
Aidha, ameeleza kuwa kitendo cha waumini hao kuingia katika makanisa mengine na kutoa mahubiri ya kuchochea ni kinyume cha sheria, na kwamba serikali haitavumilia tabia hiyo.
Amesisitiza kuwa vibali vya waumini wa Gwajima vimesitishwa na kwa sasa hakuna ruhusa kwa mikusanyiko yao yoyote.
Msando ametoa wito kwa bodi ya wadhamini wa kanisa hilo kufuta maagizo yanayohamasisha mikusanyiko haramu, huku akimtaka kiongozi mkuu wa kanisa hilo kujitokeza kwa mazungumzo ya amani ili kutafuta suluhisho la kudumu.
“Waumini wengine wa makanisa wafate kanuni na taratibu za kuabudu. Serikali haina nia ya kuzuia haki za kuabudu, bali tunataka taratibu zifuatwe,” amesema.

