WAPI heshima kwa Mbwana Samatta? Siioni. Napita mitandaoni na napita katika vijiwe, lakini siioni heshima ambayo anastahili kupewa. Michuano ya Afcon inaendelea kule Morocco na maelfu ya Watanzania wanaongea vibaya kuhusu Samatta
Desemba, mwaka huu alitimiza miaka 33. Yupo katika siku za mwisho za kucheza katika ubora wake. Samatta hayupo katika ubora wake, lakini hata Cristiano Ronaldo hayupo katika ubora wake. Lionel Messi hayupo katika ubora wake.
Mambo hufika mwisho. Yanapofika mwisho huwa tunajadili walichowahi kufanya katika mpira na tunakiheshimu kuliko viwango vyao. Kwa hiyo tunajaribu KUSAMEHE kinachoendelea na kujaribu kukumbuka kikubwa walichotufanyia. Na Samatta ndivyo alivyopaswa kujadiliwa.
Ukienda mitandaoni kwa sasa ni zile kauli zinazoudhi na kulenga kumdhalilisha Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi ya Mabingwa wa ULAYA. Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ENGLAND. Mtanzania wa kwanza kufunga bao WEMBLEY. Mtanzania wa kwanza kuifunga MANCHESTER CITY. Mtanzania wa kwanza kuifunga LIVERPOOL.
— Legend, Edo Kumwembe.
