
Fadlu Davids Kocha Mpya Yanga, Apewa Mikoba ya Manqoba Mngqithi!
Klabu ya Yanga usiku wa kuamkia leo Novemba 7, 2026 imemtangaza rasmi kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids, kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Manqoba Mngqithi ambaye ameachana na klabu hiyo kufuatia mwenendo usioridhisha wa matokeo.
Davids mwenye umri wa miaka 45 anarejea nchini Tanzania baada ya kuondoka katika klabu ya Raja Athletic Club ya Morocco, safari hii akiwa na jukumu la kuiongoza Yanga, klabu ambayo ni mpinzani mkubwa wa Simba SC, aliyowahi kuitumikia hapo awali.
Kocha huyo anarejea katika mazingira anayoyafahamu vizuri kutokana na uzoefu alioupata wakati akiinoa Simba SC, jambo linalompa uelewa wa kutosha kuhusu ushindani wa soka la Tanzania, hususan dabi ya Kariakoo inayozikutanisha klabu hizo kongwe.
Uteuzi wa Davids unatarajiwa kuongeza ushindani ndani ya kikosi cha Yanga, huku mashabiki wa klabu hiyo wakitarajia kuona mabadiliko katika mbinu za uchezaji na matokeo ya timu hiyo katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Uzoefu wake katika soka la Afrika Mashariki pamoja na historia yake ya kufanya kazi katika mazingira yenye ushindani mkubwa ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwa muhimu katika jukumu lake jipya.
Sasa macho ya mashabiki wa Yanga yanaelekezwa kwa Davids kuona namna atakavyokabiliana na changamoto ya kuendeleza mafanikio ya klabu hiyo, kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na kuipa timu ushindani katika michuano ya kimataifa.
Safari yake mpya inaanza Jangwani, lakini safari hii akiwa upande wa pili wa Kariakoo!
