KUTOKANA na Mfungo Mtukufu wa Ramadhani baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu hula tende wakati wa kufuturu.Tende ni tunda maarufu sana duniani.
Wakati huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, matumizi yake huongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu niliyoitaja hapo juu.
Lakini pengine ni vizuri kujua siri ya kupendwa na kujua lina faida gani katika mwili wa binadamu.
Wanasayansi wa masuala ya vyakula wamelifanyia utafiti tunda hili na kugundua kwamba sifa yake kubwa ni kuwa chanzo kikubwa cha kirutubisho cha nishati ya mwili (energy). Mtu ukila tende mwili huweza kupata nguvu mara moja.
Hivyo ni wazi kwamba waumini wanaofunga mchana kutwa wanahitaji kula vyakula vya kurejesha virutubisho na nishati mwilini ambayo vilikosekana kwa siku nzima.
Kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha nishati, mtu anaweza kuendelea kuishi kwa kula tende na maji tu. Tunaelezwa kuwa tende ina virutibisho muhimu visivyopungua kumi, vikiwemo Calories, Calcium, Protini asilimia 2.5, Potassium, Magnesium, Phosphorous Vitamin A na B complex na C, Folate, Carbohydrates ambavyo vyote ni muhimu kwa kinga na ustawi wa mwili wa binadamu.
Imeelezwa na wataalam kuwa tende ina kiwango kikubwa cha kamba-lishe Fibre ambazo ni muhimu kwa ulainishaji wa chakula na kuwezesha kupatikana kwa choo kirahisi kama kilikuwa kimefunga na huboresha mfumo wa fahamu.
Aidha, tende imegundulika kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya saratani ya tumbo Colon Cancer. Pia ina uwezo wa kuimarisha afya ya moyo na kuukinga na maradhi mengine kwa kunywa juisi yake ambayo hutengenezwa kwa kulowekwa.
Tende huweza pia kutibu magonjwa ya tumbo, kujaa gesi. Kwa walevi wa kupindukia, tende huweza kuondoa sumu katika miili yao.
Stori na Elvan Stambuli, Global Digital
