Kesi ya Geoffrey Mwambe na Polisi Inasikilizwa Leo Kisutu

Leo, Jumatatu Desemba 15.2025, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam majira ya saa 03 asubuhi inatarajiwa kusikiliza maombi Na. 289778/2025 yaliyofunguliwa na Waziri wa zamani Geoffrey Mwambe dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO DSM)

Maombi hayo ambayo yamefunguliwa Mahakamani hapo na Mwambe kupitia Wakili wake Hekima Mwasipu yanatarajiwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Gwantwa Mwankuga

Mwishoni mwa juma lililopita, Wakili Mwasipu aliieleza Jambo TV kuwa mteja wake amekuwa akishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Kigamboni, DSM tangu Desemba 07 mwaka huu, lakini mpaka sasa hajapewa dhamana licha ya kuwa Wakili wake alielezwa kuwa mteja wake anashtakiwa kwa uchochezi kosa ambalo linadhaminika

“Nilipewa taarifa na familia hiyo tarehe 07, na nikapata nafasi ya kuongeanae face to face huko Kituo cha Polisi Kigamboni na anatuhumiwa kwa uchochezi, na alihojiwa kwa uchochezi tu sasa tukaendelea kufanya consultation na wanaomshikilia kwaajili ya dhamana lakini kidogo mazingira hayakuwa rafiki ndio maana mpaka leo anashikiliwa” -Wakili Mwasipu

Hata hivyo, taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro Desemba 12 mwaka huu, ilieleza kuwa Jeshi hilo linamshikilia Mwambe kwa tuhuma za jinai ambazo zinachunguzwa

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi lilisema kuwa lilimkamata Mbunge huyo wa zamani wa Masasi usiku wa Desemba 07.2025 eneo la Tegeta, Kinondoni, Dar es Salaam huku likibainisha kuwa hatua kali za kisheria dhidi yake zinakamilishwa.

Related Posts