Geofrey Mwambe Anatuhumiwa Kutaka Kumuua Mkuu wa Polisi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu Desemba 15, 2025, imeyaondoa rasmi maombi namba 289778/2025 yaliyokuwa yamewasilishwa na Waziri wa zamani, Geoffrey Mwambe, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO DSM).

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi, Gwantwa Mwankuga, baada ya Wakili wa Mwambe, Hekima Mwasipu, kuwasilisha maombi ya kuyaondoa madai hayo mahakamani. Wakili Mwasipu alieleza kuwa sababu kuu ya hatua hiyo ni mteja wake tayari kupatiwa dhamana, hali iliyofanya msingi wa kuendelea na maombi hayo kukosa umuhimu kwa wakati huu.

Kwa mujibu wa Wakili Mwasipu, Mwambe alipatiwa dhamana siku ya Alhamisi, Desemba 14, 2025, hatua iliyokubaliwa na upande wa Jamhuri bila kupinga. Kutokana na hilo, Mahakama iliridhia hoja hiyo na kuamuru kufutwa rasmi kwa maombi yaliyokuwa yakiendelea kusikilizwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uamuzi huo, Wakili Mwasipu alisema kuwa mteja wake amekuwa akihojiwa kuhusiana na tuhuma mbili tofauti. Alifafanua kuwa kosa la kwanza linahusisha madai ya kupanga njama za kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, huku kosa la pili likiwa ni uchochezi unaodaiwa kufanywa kupitia mitandao ya kijamii.

Wakili huyo alieleza kuwa, baada ya kupatiwa dhamana, yeye pamoja na mteja wake walitekeleza masharti yote waliyopewa na vyombo vya usalama. Alisema leo saa 3:00 asubuhi waliripoti katika Kituo cha Polisi kama walivyoelekezwa, na baadaye wakaelezwa warejee tena kituoni hapo baada ya siku saba kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.

Aidha, Wakili Mwasipu alisisitiza kuwa licha ya dhamana hiyo, upelelezi dhidi ya Mwambe bado unaendelea, hivyo mteja wake anatakiwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola hadi pale uchunguzi utakapokamilika. Aliongeza kuwa hatua ya kuondoa maombi Mahakamani Kisutu haimaanishi kumalizika kwa kesi au tuhuma, bali ni uamuzi wa kisheria uliotokana na mabadiliko ya mazingira ya shauri hilo.

Kwa upande wake, upande wa Jamhuri haukuwasilisha pingamizi lolote dhidi ya ombi la kuyaondoa maombi hayo, hali iliyochangia Mahakama kufikia uamuzi wake kwa haraka bila mvutano wa kisheria.

Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na wananchi kutokana na uzito wa tuhuma zinazomkabili Mwambe, hasa ikizingatiwa nafasi mbalimbali za uongozi alizowahi kushika serikalini. Hata hivyo, Mahakama imesisitiza kuwa mchakato wa kisheria utaendelea kufuatwa kwa mujibu wa sheria, huku haki za pande zote zikilindwa.

Kwa sasa, macho ya wengi yanaelekezwa kwenye hatua zinazofuata za upelelezi, pamoja na uamuzi wa vyombo vya mashtaka endapo wataona kuna sababu za kuendelea na hatua za kisheria dhidi ya mtuhumiwa au la.

Related Posts