
Rayvanny amegeuza Tetema kuwa “brand” inayozalisha rekodi kila inapoguswa. Ndani ya siku nne tu, ameweka rekodi mpya kwenye YouTube Music kwa kufikisha monthly audience milioni 10.9, akimvuka Diamond Platnumz aliyewahi kushikilia rekodi ya milioni 10.2. Wasikilizaji wa Rayvanny wameongezeka kutoka milioni 4.88 ndani ya siku tatu tu, hiyo siyo kupaa, ni kuruka kama roketi.
Ujio wa Oh Mama! Tetema akishirikiana na Nora Fatehi, Vishal Mishra na Shreya Ghoshal umepokelewa kama keki mpya iliyotoka jikoni, kila mtu anataka kipande chake. Video yake ilitazamwa zaidi ya mara milioni 7.4 ndani ya saa 24 za kwanza, ikiongoza dunia nzima.
Hii siyo tu stori ya wimbo, ni mfano halisi wa jinsi muziki wa Tanzania unavyozidi kuchanja mbuga kimataifa. @Rayvanny ameonyesha kwamba “remix sahihi” inaweza kuchanganya tamaduni na mashabiki wa aina tofauti mbili duniani hadi kuleta mlipuko wa namba kwenye majukwaa yote. Hata Spotify, monthly listeners wake wamepaa kutoka 403,900 hadi 603,700 ndani ya siku 4 tu.
Kwa ukuaji huu, na ambavyo ‘Oh Mama Tetema’ inaendelea, Rayvanny anaweza kumaliza mwezi Agosti akiwa na wasikilizaji wa YouTube zaidi ya milioni 20 akiweka rekodi nyingine kubwa zaidi.
Kifupi, Tetema imegeuka injini ya rekodi, na Rayvanny ndiye dereva wa mashindano haya ya muziki wake duniani.

