
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, limetangaza kuwa limekubali rasmi pendekezo la kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili katika vita vinavyoendelea, hatua inayotazamwa kama nafasi ya kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na kupunguza mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika taarifa yake rasmi, Baraza hilo limesisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi mwisho wa vita, likieleza kwamba sitisho hilo ni la muda na lina lengo la kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani kuendelea.
“Inasisitizwa kwamba hii haimaanishi kumalizika kwa vita,”
imesema taarifa ya Baraza hilo.
Iran imeongeza kuwa vikosi vyake vya ulinzi bado viko tayari kujibu shambulio lolote kutoka kwa upande wa adui, ikisema kuwa “mikono yetu bado ipo kwenye kichochezi”, ishara kwamba nchi hiyo bado iko katika hali ya tahadhari ya juu ya kijeshi.
Hatua hii inafuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alisema Marekani itasitisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa muda wa siku 14, kwa masharti ya kufunguliwa kwa njia ya bahari ya Strait of Hormuz na kuendelea kwa mazungumzo ya amani.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema hatua hii inaweza kuwa mwanzo wa makubaliano mapana ya amani, ingawa kauli ya Iran inaonyesha wazi kuwa hali bado ni tete na vita vinaweza kuendelea ikiwa mazungumzo hayatatoa suluhisho la kudumu.
