Jenerali Muhoozi Atamani Kumuua Bob Wine, Adai Amteua Wanachama Wake 22

UGANDA – Kauli zilizochapishwa mtandaoni na Mkuu wa Majeshi ya Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, zimeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi hiyo, baada ya kuhusishwa na matamshi yanayotafsiriwa kama vitisho dhidi ya Kiongozi wa upinzani na Rais wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi alichapisha jumbe kadhaa zenye lugha kali, akidai kuwepo kwa mauaji ya wanachama wa NUP na kuashiria nia ya kumdhuru Bobi Wine, ambaye katika baadhi ya jumbe hizo alimtaja kwa jina la “Kabobi”.

Miongoni mwa jumbe zilizochapishwa, Muhoozi alidai kuwa tangu wiki iliyopita watu 22 anaowataja kama “magaidi wa NUP” waliuawa, huku akitamani mhanga mwingine awe Bobi Wine. Katika ujumbe mwingine, alitoa kauli ya kutishia kuwaua papo hapo wanachama wanaojiita “Foot Soldiers” wa chama cha NUP hadi pale “Mzee” atakapoelekeza vinginevyo.

Baadhi ya jumbe hizo baadaye zilifutwa, hata hivyo zilikuwa tayari zimesambaa kwa kasi mitandaoni na kunakiliwa na watumiaji mbalimbali.

Katika kauli hizo pia, Muhoozi alijitambulisha kama “nabii wa Mungu” na kudai kuwa alitabiri ushindi mkubwa wa Rais Yoweri Museveni katika chaguzi zilizopita, huku akidai kuwa chama cha NUP kitaondolewa kabisa katika ulingo wa kisiasa wa Uganda.

Si mara ya kwanza kwa Jenerali Muhoozi kuibua taharuki kupitia matamshi yake ya mitandaoni. Amekuwa akijulikana kwa kutoa kauli zenye utata zinazogusa masuala ya upinzani, masuala ya kijeshi na siasa za kimataifa, hali inayowafanya wachambuzi wengi wa siasa kuhoji iwapo kauli hizo ni maoni yake binafsi au zinaakisi msimamo rasmi wa dola ya Uganda.

Hadi sasa, Serikali ya Uganda haijatoa tamko rasmi la kufafanua wala kujibu kauli hizo, huku chama cha National Unity Platform (NUP) kikiendelea kulalamikia kile kinachokiita vitisho, ukandamizaji na matumizi ya nguvu dhidi ya wafuasi wake.

Related Posts