
Mbunge Mteule wa Viti Maalum Kundi la Vijana (CCM), Mkoa wa Geita Jesca Magufuli @jesca.jmagufuli amemkaribisha Chato, Mgombea Urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo amesema kuwa Wanachato wamejitokeza kwa wingi kutokana ahadi aliyoitoa wakati wa mazishi ya Dkt. Magufuli ambapo aliahidi ya kuwa hatowaacha wananchi wa Chato.
Akizungumza mbele ya Mgombea Urais Dkt. Samia katika Mkutano wa Kampeni za Uchaguzi, uliofanyika Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita hii leo Octoba 13, 2025 amesema kuwa utekelezaji wa miradi uliofanyika chini ya Dkt. Samia ni dhahiri kuwa Dkt. Magufuli hakufanya kosa kumchagua ambapo pia amewaomba Wananchi wa Chato kumpigia kura Dkt. Samia ili akaendelee kuleta miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Chato.
“Na hakika hili umeweza kulidhihirisha mama na mimi leo niko mbele yenu wazazi wangu lakini niko mbele hapa nikiongea katika ardhi ambayo amelala mzee wangu wanachato mama tunakupenda sana, leo tunajivunia kwa miradi mikubwa ambayo imeweza kufanyika hapa kwa hiyo ndugu zangu tutangulize utanzania wetu mbele lakini pia tuweze kushukuru kwa yale yote ambayo tumefanyiwa na Dkt. Samia na hii inaonesha wazi kwamba mzee wetu Dkt. Magufuli hakufanya makosa kukuchagua wewe mama yetu” Amesema Jesca.

