Jeshi la Polisi: Hakuna Maandamano Video Zinazosambaa ni za Zamani

Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari hadi kufikia mchana wa Desemba 9, 2025, siku ambayo baadhi ya watu wamepanga kufanya maandamano yanayodaiwa kuwa ya amani, huku Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vikisema maandamano hayo si halali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuimarisha hali ya usalama na kulinda maisha na mali za wananchi kote nchini.

Polisi imewataka wananchi kupuuza picha mnato na picha mjongeo zinazoenezwa mitandaoni zikidai kuwa maandamano yameanza sehemu mbalimbali za nchi, ikibainisha kuwa picha hizo ni za matukio ya zamani zikiwemo zile za Oktoba 29, 30 na 31, 2025.

DCP Misime amesema baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakitumia video za zamani kujaribu kupotosha umma, akitaja mfano wa tukio la Juni 2025 ambapo jamii ya Wamasai walikuwa wakifanya sherehe za jando katika msitu wa TANAPA, lakini picha hizo zikasambazwa leo zikionesha kana kwamba Wamasai wanaandamana kudai haki zao jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa taarifa hizo si sahihi na zinalenga “kuwahadaa wananchi kwamba maandamano yanafanyika”, huku akiwatoa wito Watanzania kuendelea kupuuza upotoshaji huo.

Polisi imekumbusha kuwa maandamano yaliyopewa jina la “maandamano ya amani yasiyo na kikomo” yalipigwa marufuku tangu Desemba 5, 2025 kwa kuwa hayakufuata matakwa ya kisheria, ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi sura ya 322.

Katika hitimisho la taarifa yake, DCP Misime ameendelea kuwasihi wananchi kufuata sheria na taratibu ili kulinda usalama wa wote.

Related Posts