Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limethibitisha kumshikilia Waziri wa zamani, Geofrey Mwambe, tangu usiku wa Desemba 7, 2025 alipokamatwa katika eneo la Tegeta, Kinondoni, kwa tuhuma zinazohusiana na makosa ya jinai ambayo bado hayajatajwa, yanayoendelea kuchunguzwa.
Taarifa ya polisi iliyotolewa leo Desemba 12, 2025 imeeleza kuwa Mwambe, waziri wa zamani wa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na baadaye Viwanda na Biashara, alikamatwa wakati wa operesheni ya kawaida ya ufuatiliaji wa matukio ya usalama jijini Dar es Salaam, na kwamba hatua za awali za kisheria kuhusu tuhuma hizo zinaendelea kukamilishwa.
Mwambe aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), mbunge wa Masasi, Mtwara (CCM), ameshikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 7, 2025 na baada ya kimya kutawala juu yake, jana Desemba 11, 2025 Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), walifunguliwa mashtaka mahakamani kwa kumshikilia kinyume cha sheria.
Shauri hilo la maombi namba 289778/2025 lilifunguliwa na Mwambe akiwa mwombaji kupitia kwa wakili wake, Hekima Mwasipu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya hati ya dharura na lilipangwa kusikilizwa Desemba 15, 2025.
Mbali na taarifa hiyo, Polisi imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuviachia vyombo vya dola kukamilisha taratibu za uchunguzi na hatua za kisheria.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kulitaka Jeshi la Polisi kuzingatia ukamataji wa staha na kufuata sheria za nchi.
