Jeshi la Polisi Tanzania limepiga marufuku “maandamano ya amani yasiyo na kikomo,” yaliyotangazwa kufanyika Desemba 9, 2025, likisema yamekosa sifa za kisheria na yanaashiria mipango ya uhalifu unaoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Katika taarifa iliyotolewa Desemba 5, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, jeshi hilo limesema kuwa hali ya usalama inaendelea kuimarika, huku likiwashukuru wananchi kwa ushirikiano katika kulinda amani. Hata hivyo, Polisi imeeleza kuwa ufuatiliaji wa kina umebaini mipango hatarishi inayoratibiwa mitandaoni na kupitia makundi ya watu wanaohamasisha maandamano hayo.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, maandamano hayo yamepigwa marufuku kwa misingi ya Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322, ambayo inataka mtu yeyote anayetaka kufanya mkusanyiko au maandamano kuwasilisha notisi kwa maandishi kwa Afisa Polisi Msimamizi. Hadi tarehe ya leo, hakuna taarifa yoyote ya maandishi iliyowasilishwa katika ofisi yoyote ya Mkuu wa Polisi Wilaya nchini.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchunguzi unaendelea kuonesha kuwa wahamasishaji wa maandamano hayo wanapanga mbinu mbalimbali hatarishi, ikiwemo kuwataka watu waliopata mafunzo ya silaha kuzitumia siku hiyo; kusimamisha shughuli zote za kawaida; kuchoma minara ya mawasiliano ili kukatisha huduma; kufunga barabara zinazoelekea na kutoka Bandarini Dar es Salaam; pamoja na kufunga mipaka ya nchi.
Pia, imebainishwa kuwepo kwa wito wa kupora mali za watu kwa kisingizio cha njaa, kuzuia huduma hospitalini, kuwadhuru watumishi wa serikali, kutoa vitisho vya kuuawa kwa wanaoweza kuonekana mitaani, na wito mwingine wa kubeba petroli katika chupa siku hiyo.
Polisi imesema matukio hayo yanayoendelea kupanga na kuhamasishwa ni viashiria vya wazi vya kuvunjika kwa amani, kuhatarisha maisha ya watu, kuathiri uchumi, na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi.

