Kesi ya uhaini Na. 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu inaendelea tena leo, Alhamisi Februari 12.2026 kama ilivyo ada mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru
Jana (Jumatano, Februari 11.2026), Mahakama ilitoa uamuzi mdogo wa mapingamizi matano (5) yaliyokuwa yamewekwa na mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo, ambapo manne (4) kati ya mapingamizi hayo yalitupiliwa mbali huku moja (1) likikubaliwa
Moja lililokubaliwa na Mahakama ni lile linalohusu kizimba maalum kilichojengwa kwenye chumba cha Mahakama kwaajili ya kutumiwa na mashahidi wa siri (raia), ambapo Mahakama iliagiza kizimba hicho kifanyiwe marekebisho ili Majaji waweze kumuona shahidi, sambamba na kufuatilia mwenendo wako akiwa kwenye kizimbani
Hata hivyo, Mahakama ilitoa uwanja kwa upande wa Jamhuri, kwamba endapo marekebisho ya kizimba hicho yatakuwa yamekamilika basi wanaweza kumleta shahidi wa siri kama walivyokusudia awali (kwamba shahidi wa 4 wa Jamhuri ni wa siri), na endapo marekebisho hayo yatakuwa hayajakamilika basi upande wa Jamhuri unaweza kuleta shahidi asiyekuwa wa siri (Askari) ili atoe ushahidi wake Mahakamani,
Maagizo ya Mahakama yalienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, endapo chumba namba moja (1) cha Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kinachotumika kusikilizia kesi hiyo kitakuwa bado kwenye ‘matengenezo (marekebisho ya kizimba)’ kesi hiyo haitasimama kwani kitatumika chumba kingine, miongoni mwa vyumba vilivyopo Mahakamani hapo,
‘Mpira’ sasa upo upande wa Jamhuri, je utamleta shahidi wa siri (raia) au shahidi asiyekuwa wa siri (askari) leo?, hilo litafahamika pindi kesi hiyo itakapoanza hapo baadae.
