Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kuvunjwa kwa ukuta wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uliopo pembezoni mwa barabara ya Tunduma ili ipatikane nafasi ya kupanua barabara hiyo.
Ameyasema hayo leo Desemba 17, 2025 mkoani Songwe anapofanya ziara ya kukagua uharibifu katika Mahakama ya mwanzo Tunduma ambapo amesema ameshazungumza na Kamishna Jenerali wa TRA.
Barabara hiyo inayotajwa kubeba uchumi wa Mkoa wa Songwe kwa nyakati tofauti imekuwa ikilalamikiwa kutokana na msongamano wa malori yanayoingia na kutoka nchini.
“Zoezi lianze mara moja na nilishaambiwa kuna uhitaji wa kusogeza ukuta ili kupata nafasi ya kujenga barabara nimeshaongea na TRA na amewaelekeza wasaidizi wake jambo la kuhamisha ukuta lianze mara moja.”
“Maandalizi yaanze kupanua barabara ili ziweze kupita njia tatu hadi nne mliopewa kazi muanze mara moja,” amesema.
Agizo hilo linafuatia kilio cha ufinyu wa barabara hiyo kilichowasilishwa awali na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame aliyesema msongamano wa malori unasababishwa na ufinyu wa barabara.
Pia awali Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema yalitolewa mapendekezo barabara ya njia moja ipanuliwe ziwe njia nne.
Hivyo, akitoa maagizo, Dk Mwigulu amesema hata taasisi zingine zilizopo karibu na eneo hilo pia ziitwe ili nafasi ipatikane lengo ikiwa ni kuondoa foleni ambayo imekuwa kero katika eneo hilo.
