Kocha wa Yanga Ataki Utani, Aitisha Wachezaji Watatu Wapya

Kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amekingalia kikosi cha timu hiyo kilivyo kwa sasa, kisha kuuambia uongozi wa klabu hiyo, umletee mashine mpya tatu amalize kazi.

Mabosi wa Yanga wamepokea ripoti ya kwanza ya Pedro baada ya kukisimamia kikosi hicho katika mechi sita za mashindano zikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na nne za Ligi Kuu Bara, zilizotosha kumpa picha ya wapi anataka kuiboresha mara michuano ikirudia tena

Taarifa kutoka kwa mabosi wa Yanga ni kwamba, Pedro ametaka kutafutiwa kiungo mkabaji mwenye ubora mkubwa, japo amesisitiza Duke Abuya amefanya kazi bora eneo hilo lakini anataka kumhamisha. Ripoti ya Mreno huyo inasema, endapo atapata kiungo huyo mkabaji basi Abuya atahamishwa nafasi akisogezwa juu, hatua ambayo itaifanya Yanga kuwa na ubora mkubwa eneo la katikati kutokana na uwezo wa Mkenya huyo sambamba na kiungo atakayekuja.

Ripoti hiyo pia inahitaji kiungo mshambuliaji, yaani namba 10 na bado Pedro haridhishwi saana na watu alionao eneo hilo huku akionyesha hataki kutumia fundi Pacome Zouzoua eneo hilo. Pedro ameonyesha anataka kumtumia Zouzoua kama kiungo wa pembeni akitokea kushoto akicheza eneo nusu (half space) jukumu litakalomfanya kuwa hatari zaidi mbele ya lango la mpinzani na kuinufaisha Yanga kuliko ilivyo sasa akiwa amefunga mabao mawili na asisti mbili vilevile.

Akili hiyo ya Pedro ya kutaka namba 10 inawaweka mtegoni Mamadou Doumbia na Lassine Kouma ambao walikuwa wanapewa nafasi kwa nyakati tofauti kucheza nafasi hiyo, licha ya Ecua Celestine naye kuwa mchezaji wa nafasi hiyo, japo kwa sasa anachezeshwa pembeni kama winga.

Kocha huyo Mreno pia anataka kutafutiwa winga mmoja mwenye ubora mkubwa atakayeongeza nguvu ya kuzalisha mashambulizi kutokea pembeni.

Related Posts