
Katika ulimwengu wa mahusiano ya kimapenzi, si kila mwanaume anayekuonesha ishara za mapenzi huwa na nia njema. Wengine huingia kwa tamaa, maslahi binafsi au kwa ajili ya kukidhi haja zao za muda, bila kujali hisia wala thamani ya mwanamke anayekuwa naye. Kwa hiyo, ni muhimu mwanamke kujifunza kusoma alama za onyo mapema kabla hajavunjwa moyo.
1. Akikuomba pesa mara kwa mara
Hili ni onyo kubwa zaidi ambalo wanawake wengi hulipuuza wakiwa wamelewa katika dimbwi la mapenzi. Mwanaume wa kweli, aliye na nia ya dhati, hatajenga mahusiano juu ya utegemezi wa kifedha. Kama kila mara anakutumia ujumbe au kupiga simu kukuomba hela ya vocha, chakula, mahitaji madogo au makubwa bila aibu, jua huyo si mwenza bali ni mnyonyaji. Mapenzi ya kweli hayaambatani na ulazima wa kutoa fedha mara kwa mara. Mwanamume mwenye malengo hufanya bidii kutatua changamoto zake mwenyewe kabla ya kumshirikisha mpenzi wake.
2. Akikuomba picha za faragha au za aibu
Hii ni dalili ya mwanaume ambaye hakuthamini, hana heshima kwako na anakuona kama chombo cha starehe. Mara nyingi wanaume wa aina hii hutumia picha hizo kwa malengo ya tamaa au hata kukushinikiza baadae. Wanawake wengi wamejikuta wakidhalilika mitandaoni kutokana na kuamini sana mapenzi ya uongo na kutoa picha za faragha. Mwanaume anayekupenda kweli atakulinda, ataheshimu mwili wako na hatawahi kukuomba jambo ambalo linaweza kukuumiza au kukuharibia heshima yako mbele ya jamii.
3. Akikuomba kuficha uhusiano wenu
Kama mwanaume anakupenda, hataona sababu ya kukuweka “siri”. Kukuomba usimwambie mtu kuhusu mahusiano yenu ni ishara kuwa ama ana mpenzi mwingine au hana nia ya kuwa nawe kwa muda mrefu. Mwanaume wa kweli hupenda kumtambulisha mpenzi wake, angalau kwa marafiki wa karibu au familia. Ukiona anakataa kila aina ya kutambulisha au hata kukutaja hadharani, jua huna nafasi ya kweli kwenye maisha yake – ni kama vile unaficha ushahidi wa uhalifu!
Mapenzi ya kweli yanajengwa kwenye heshima, uaminifu na uwazi. Kama mwanaume anakuonesha tabia hizi tatu kwa namna yoyote – anakudanganya, anakutumia au anakuchezea. Usipoteze muda, jiheshimu na tafuta mtu anayekupenda kwa dhati.
Je, umewahi kukumbana na mwanaume wa aina hii? Toa maoni yako hapo chini. Share makala hii uwasaidie wanawake wengine kutambua mapema na kuepuka wanaume wa aina hii.
