
Mwanachama wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amesema matamanio yake makuu ni kuona anaruhusiwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuonesha utofauti wa kampeni baina ya vyama vingine na kutimiza kusudio lake la kuongoza nchi baada ya kushinda uchaguzi, akibainisha kuwa Taifa linahitaji viongozi wa aina yake.
Ameyasema hayo leo Oktoba 06, 2025 nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu Dodoma) mara baada ya kusikilizwa kwa Shauri la Kikatiba Na. 24027 la mwaka 2025, analopinga kuondolewa kugombea nafasi hiyo dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mahakama hiyo, chini ya jopo la majaji watatu—Jaji Frederick Manyanda, Jaji Sylvester Kainda na Jaji Abdallah Gonzi—imepanga kutoa hukumu ya shauri hilo Oktoba 10, 2025 saa 8:00 mchana.
Katika hatua ya leo, Mahakama ilijiridhisha kuhusu utekelezaji wa amri ya kuwasilisha hoja kwa maandishi kutoka pande zote kabla ya kutangaza tarehe ya hukumu.

