Na; mwandishi wetu
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi imeagiza aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, na Naomi Raymond Kwayu (Fainess Dawson Kiwia) kumlipa Johnsen Leonard Mahururu Shilingi za Kitanzania Bilioni tatu, na milioni mia mbili ishirini (Tsh. 3,220,000,000/-) kama fidia za uharibifu baada ya kubomoa kimakosa jengo lake alilokuwa amejenga katika kiwanja namba 484 (2196) kilichopo Block H, Mbezi Africana jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo umetolewa tarehe 21/01/2026 na Jaji Sharmillah Sarwatt Kazi katika kesi ya ardhi Na. 000032646 ya mwaka 2024 iliyofunguliwa na Johnsen Leonard Mahururu dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na wenzake sita (6) ambapo imeelezwa kuwa uamuzi wa kubomoa jengo la makazi na jengo la Hoteli uliofanyika tarehe Machi 01, 2024 kwa maagizo ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa kwa madai kuwa kiwanja kile ni mali ya Naomi Raymond Kwanyu haukuwa sahihi kwani Mahururu ni mmiliki halali wa kiwanja hicho
Katika maamuzi yake, Mahakama imemtambua Mahururu kama mmiliki halali wa kiwanja hicho kutokana na kile kilichoonekana kuwa alinunua kwa mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Juma Rajabu Kapungu Januari 31, 2022, ambapo Kapungu alinunua kiwanja hicho kwa kwa kampuni ya Wood Pecker Company Limited Februari 13,1997
Baada ya kusikiliza hoja za wadaawa wote, Mahakama imemuagiza Msajili wa Hati kumfutia hati Naomi Kwayu na mleta maombi ambaye ni Mahururu kupewa hati hiyo, huku ikiamuru kuwa Mahururu atalipwa Shilingi za Kitanzania bilioni 3.18, na kwa kuvunjiwa nyumba ya makazi ambayo ilijengwa kihalali na ilikuwa na kibali cha ujenzi
Pia Mahakama imesema mleta maombi atalipwa shilingi milioni 40 kama gharama za uharibifu wa jumla na atalipwa gharama za kesi, gharama ambazo zitalipwa na Manispaa ya Kinondoni, Jerry William silaa na Naomi Raymond Kwayu (Fainess Dawson Kiwia)
Pamoja na hayo jengo la Hoteli ambalo aliomba kulipwa fidia ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 16.24 hatolipwa kwani hakuwa na kibali cha ujenzi.
